Baraza la mji wa Eldoret yapanga kuweka mapipa ya taka kwenye mabarabara ya mji.
Baraza la manispaa ya mji wa Eldoret linapanga kuweka mapipa ya kutupa taka kwenye barabara za mji huo. Meya wa mji wa Eldoret Samuel Ruto alisema baraza hilo pia limetenga sehemu tofauti za kuvutia sigara mojawao ikiwa sehemu iliyoko karibu na mto wa Sosiani. Wakati uo huo Meya Ruto alikanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa baraza lake linawafurusha makahaba kutoka katikati mwa mji haswa katika msimu huu wa mavuno unaohusishwa na ovu hilo akisema zoezi hilo limekuwa likiendelea na lilikusudiwa kusafisha mji. Akiungwa mkono na madiwani wenzake meya huyo aliwashauri wakulima kutumia pesa zao kwa busara na kuepukana na vibiriti ngoma wanaotoka kwenye sehemu mbalimbali za humu nchini kwa madhumuni ya kuwalaghai. Baraza la mji wa Eldoret limeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha usafi wa mji ikiwemo kupanda maua na kupaka rangi nyumba.
Mwisho……..Carolyne Koech