Waliotarajiwa kunufaika na bidhaa za ukulima walalamika
Zaidi ya wakulima elfu tatu katika eneo la Turbo waliopangiwa kunufaika na pambajeo za bure za ukulima kutoka kwa serikali wameiomba serikali kuharakisha utoaji wa bidhaa hizo kabla ya msimu wa upanzi wa mahindi kuisha. Wakiongozwa na mwakilishi wao David Ngenda wakaazi hao ambao wengi wao ni waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wanadai kuwa pambajeo hizo zilikuwa zikiuzwa na hivyo kupelekea wengi wao kukosa kuzipata kwani hawangeweza kumudu bei huku wakielekezea kidole cha lawama machifu. Ngenda anadai kuwa walijaribu kukutana na mkuu wa wilaya ya Eldoret magharibi ili kumpa malalamishi yao walakini hawakufaulu. Vile vile wamesema kuwa walichukua hatua ya kukutana na mkuu wa mkoa wa bonde la ufa ambaye aliwaahidi kushughulikia jambo hilo walakini wanadai kuwa wiki mbili zimepita bila ya jawabu kutolewa na utawala wa mkoa. Kwa sasa wakulima hao wanahofia kupitwa na msimu wa upanzi ikiwa maswala yao hayatasuluhishwa kwa dharura.
Mwisho…………..Carolyne Koech